UTABIRI WA MSIMU WA MASIKA (OKTOBA – DISEMBA, 2020) WILAYA YA MVOMERO, MKOA WA MOROGORO

Taarifa hii inatoa mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli katika kipindi cha Oktoba – Disemba, 2020 na athari zake kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi katika Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro

Dondoo muhimu
• Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika Wilaya ya Mvomero. Kwa kawaida wastani wa mvua katika miezi ya Oktoba – Disemba ni kati ya milimita 300 hadi 500 kwa baadhi ya maeneo ya kaskazini-mashariki na milimita 200 hadi 300 kwa maeneo mengine yaliyosalia.
• Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2020.
• Hali ya upungufu zaidi wa mvua inatarajiwa hususan katika maeneo ya kati ya Wilaya ya Mvomero kuelekea Kusini ukilinganisha na maeneo ya Kaskazini.
• Vipindi vya ukavu vinatarajiwa katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba na wiki ya kwanza ya mwezi Disemba, 2020.
• Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2021.

Mvua za Msimu wa Vuli (2020) kwa Wilaya ya Mvomero
Zitaanza: Katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2020.
Zitaisha: Mwezi Januari, 2021.
Urefu wa Msimu: Kiujumla unatarajiwa kuwa mfupi kwa kipindi cha Oktoba – Disemba, 2020.
Kiasi cha mvua zinazotarajiwa: Chini ya wastani hadi wastani.
Kiwango cha juu cha mvua: Kinatarajiwa katika wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2020.
Vipindi vya ukavu: Upo uwezekano wa kutokea vipindi vifupi vya ukavu kati ya wiki ya kwanza ya mwezi Novemba na wiki ya kwanza ya mwezi wa Disemba, 2020.
Mtawanyiko: Mvua zinatarajiwa kuwa na mtawanyiko wa kutoridhisha katika maeneo mengi ukilinganisha na msimu wa Vuli uliopita wa 2019.

Angalizo:
­ Watumiaji wa taarifa hii wanashauriwa kufuatilia utabiri wa siku 10, saa 24 pamoja na tahadhari kila zinapotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

­ Wakulima, wafugaji na wavuvi wanashauriwa kupata ushauri zaidi kutoka kwa maafisa ugani kwa matumizi sahihi ya taarifa za utabiri wa hali ya hewa.

Matokeo na ushauri kwa kilimo, mifugo na uvuvi
Matokeo
o Kunatarajiwa kuwa na upungufu wa unyevunyevu katika udongo kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo.
o Magonjwa na wadudu waharibifu yataweza kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upungufu wa unyevunyevu hata hivyo, wadudu kama mchwa wataongezeka kutokana na upungufu wa mvua.
o Upungufu wa maji kwenye mabwawa na mito vinatarajiwa hivyo kuathiri upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, umwagiliaji na chakula cha samaki.
o Migogoro kati ya wakulima na wafugaji inaweza kujitokeza kutokana na upungufu wa rasilimali maji na malisho.

Ushauri
o Wakulima kutumia mbegu bora zinakomaa mapema na kuvumilia ukame kama vile mihogo, mikunde na mahindi aina ya katumani na kito.
o Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu za kilimo hifadhi kama vile matumizi ya matuta ya kufunga na kilimo mseto kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa unyevunyevu unaotarajiwa.
o Wafugaji na wakulima wanashauriwa kutumia teknolojia ya uvunaji maji ya mvua kwa matumizi ya baadae.
o Wafugaji wanashauriwa kutumia maji na malisho kwa uangalifu ili kukabiliana na upungufu unaotarajiwa ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

Utabiri wa hali ya hewa nchini na tahadhari zinapatikana katika tovuti ya Mamlaka: www.meteo.go.tz

Mawasiliano yote yaelekezwe kwa:
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Morogoro Rd, Ubungo Plaza, Ghorofa ya 3,
S.L.P. 3056, Dar es Salaam, Tanzania. Nukushi: +255 22 2460735, Simu: +255 22 2460706-8.
Barua pepe: met@meteo.go.tz, Tovuti: www.meteo.go.tz
(IMETHIBITISHWA – ISO 9001:2015, Huduma za Hali ya Hewa kwa Usafiri wa Anga)

You can also download the PDF form of this below
Pia unaweza kupakua utabiri huu hapo chini

Mvomero_ 2020_Final

Post a comment